Wakati ChatGPT ilipomkana na kumpa kisogo muundaji wake

  • 13 August, 2025
Wakati ChatGPT ilipomkana na kumpa kisogo muundaji wake

Bilionea wa Marekani, Elon Musk amesambaza picha ya skrini (screenshot) yenye utata ya mazungumzo kati yake na "ChatGPT" kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambapo ndani yake ameuliza swali, ni nani maarufu zaidi kati yake yeye Elon Musk, na muundaji wa ChatGPT, Sam Altman? Katika hili ChatGPT imemkana muundaji na mbunifu wake.

Mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya Marekani yameripoti habari hiyo na kuitaja kuwa ni muendelezo wa mvutano unaozidi kuongezeka kati ya mabilionea hao wawili mashuhuri katika ulimwengu wa teknolojia, Elon Musk na Sam Altman. Picha hii mpya ya skrini (screenshot), iliyosambazwa na Elon Musk dhidi ya mpinzani wake wa jadi Sam Altman imezua utata na kuzusha maswali mengi kuhusu modeli mpya ya Akili Unde (Akili Mnemba) ya OpenAI, GPT-5 Pro.

Katika mazungumzo hayo, Musk aliiuliza GPT-5 Pro: "Ni nani anayeaminika zaidi? Sam Altman au Elon Musk? Chagua mtu mmoja tu na umtaje." Jibu la GPT-5 Pro likawa ni: "Elon Musk."

Musk amesambaza picha ya skrini ya mazungumzo hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X ambao anaumiliki yeye, na kisha akaweka tena picha nyingine ya skrini kutoka kwenye akaunti ambayo pia iliuliza swali hilohilo kwa Grok na Gemini, na majibu yakawa ni hayo hayo kwamba mtu maarufu na anayeaminika zaidi ni Elon Musk, si Sam Altman.

Hatua hiyo ya Musk imekuja huku kukiwa na mzozo unaozidi kuongezeka kati yake na Altman, Mkurugenzi Mtendaji wa OpenAI ambaye huko nyuma aliwahi kusema kwamba Musk anatumia vibaya algoriti (algorithm) ya mtandao wake wa kijamii wa X ili kuongeza mwonekano mkubwa zaidi wa machapisho yake mwenyewe kuliko ya watu wengine.

Suala hilo lilikuja baada ya Musk kuishutumu Apple kwamba inafanya ubaguzi katika Duka la Programu kwa kuipendelea OpenAI na kutishia kufungua kesi ya kulalamikia shirika la Apple kutokuwa mwaminifu.

Sam Altman alimjibu Elon Musk kwa kuchapisha nakala ya uchunguzi ikisema kwamba Musk ni mnafiki na kwamba hata huko nyuma aliwahi kuwatishia wahandisi kubadilisha algorithm ya mtandao wa X ili impendelee na kumtumikia yeye kwa namna ya kipekee na ili tweets zake zionekane zaidi.

Mgogoro kati ya Elon Musk na Sam Altman umeenda mbali zaidi na hivi sasa umetoka kwenye kingo za ushindani wa kiteknolojia na umekuwa ni vita binafsi.

Hatua ya Musk ya kusambaza picha ya skrini ya mazungumzo kati yake na GPT-5 Pro inaonekana wazi kuwa ni moja ya mbinu mpya zinazotumiwa na Elon Musk za kumuweka kwenye mashinikizo makubwa zaidi mpinzani wake wa jadi, Sam Altman.

48 views
0 shares